Ijumaa, 17 Aprili 2015

Matukio Yanayoelezea Kurudi kwa Bwana Yesu Kristo

senior pastor Francis Mhina
Kurudi kwa Yesu Kristo duniani ni sehemu ya mpango wa Mungu kuhusu wokovu wa wanadamu na pia ni swala linalozungumziwa sana katika vizazi mbalimbali. Hata mtume Petro alimuuliza Yesu Kristo swali hili miaka elfu mbili iliyopita. “Tuambie, mambo hayo yatakuwa lini? Nayo ni nini dalili ya kuja kwako, na ya mwisho wa dunia” (Mathayo 24:3). Katika kulijibu swali hili, Yesu hakutaja mwaka, siku wala saa, badala yake alielezea dalili zitakazotokea kabla ya siku hii kuu ya kurudi kwake.
Mtume Petro, Paulo na mwinjilisti Luka waliandika kwa kina kuhusu dalili hizi. Hata Yohana katika kitabu chake cha ufunuo wameandika kwa mapana kuhusu dalili hizi. Kwa kuelezea dalili hizi, Biblia imewatoa wanadamu katika giza la kutotambua majira ya kurudi kwa Yesu Kristo. Kuanzia kitabu cha Mwanzo mpaka kitabu cha Ufunuo wa Yohana yako maelezo mengi kuhusu nyakati za mwisho na kurudi kwa Yesu Kristo. Maandiko haya yanaonyesha wazi kuwa habari za kurudi kwa Yesu ndicho kiini cha mpango wa Mungu wa wokovu kwa wanadamu Wasomi wa Biblia wamegundua kwamba katika kila aya thelathini katika Biblia takatifu, aya moja inazungumzia juu ya kurudi kwa Yesu. Kinachoonekana hapa ni kuwa kurudi kwake kumeelezewa mara nyingi zaidi kuliko kuja kwake kwa mara ya kwanza.
Katika Agano la Kale kurudi kwa Bwana kunatajwa mara kwa mara katika vitabu vya manabii, na katika Agano Jipya ziko sura maalum zinazozungumzia swala hili. Kutajwa huku kunaonyesha jinsi kuzaliwa kwa Kristo na kazi yake ya ukombozi, kulivyotabiriwa maelfu ya miaka kabla ya kutokea. Tunachojifunza kutokana na ukweli huu ni kuwa, yote yaliyotabiriwa katika Biblia kuhusu kurudi kwa Mwana wa Mungu na mwisho wa dunia kutatokea bila shaka yoyote. Katika Biblia tunasoma haya: “Huyu Yesu aliyechukuliwa kutoka kwenu kwenda juu mbinguni, atakuja jinsi iyo hiyo mlivyomwona akienda zake mbinguni” (Matendo ya Mitume 1:11).
Unabii huu ndio ujumbe mkubwa katika nabii za Mungu, na ni ukweli unaogusa mioyo ya wanadamu wote na kuwaletea matumaini wakati wa mashaka, na kukosa raha. Swali kubwa tunaloweza kujiuliza kuhusiana na unabii huu wa kurudi kwa Yesu, ni hili la ni lini tukio hili litakapotokea? Mkristo wa kweli anayefahamu Neno la Mungu hatathubutu kubashiri saa, siku au mwaka ambao mwisho wa dunia na hukumu ya mwisho vitatokea. Ufunuo pekee tulio nao ni maneno yaliyotamkwa na Yesu pale aliposema kuwa, “Si kazi yenu kujua nyakati wala majira, Baba aliyoyaweka katika mamlaka yake mwenyewe” (Matendo ya Mitume 1:7). Hata hivyo kutokana na umuhimu wa mambo haya kwa kila wanadamu, Yesu Kristo hakuwaacha wanafunzi wake katika giza kuhusu siku hii ya hukumu na ya kurudi kwake. Katika Biblia tunasoma juu ya hali na matukio mbalimbali yatakayotokea duniani yanayojulikana katika Biblia kama dalili za siku mwisho.

Kutokea kwa nyakati za dhiki

Miongoni mwa dalili za siku za mwisho ni pamoja na vita, kuongezeka kwa maasi, magonjwa, njaa, matetemeko ya ardhi,ukatili, chuki, kuporomoka kwa maadili, uzushi, uongo, kutawaliwa na pesa, ukaidi, kuharibu mimba, kutowajali wengine, ugaidi, tawala mbaya na maovu mengine yanayofanana na haya. Katika miaka tuliyo nayo mambo haya yameenea kama mafuriko ukilinganisha na ilivyokuwa huko nyuma. Kutokana na mafuriko haya ya maovu na majanga, walimwengu wanayaona mambo haya kama kitu cha kawaida.

Dalili kupotoka kwa wanadamu kiroho

Yesu alitabiri pia kuhusu mafundisho ya uongo pamoja na walimu watakaopotosha mafundisho ya kweli ya Yesu Kristo. Wakati huo huo alitabiri kuhusu kuongezeka kwa chuki dhidi ya wanafunzi wa kweli wa Yesu Kristo. Biblia imeeleza bayana kuwa wakristo watateswa katika nchi mbalimbali. Siku hizi tunashuhudia jinsi watu wanavyopotoshwa kiroho kwa njia mbalimbali. Leo hii kuna dini zinazoshughulikia imani za siri zinazomkataa Mungu huku kukiwa na ongezeko kubwa la watu wanaojihusisha katika mambo ya uchawi, nyota, mizimu, kuangalia nyakati mbaya na mafundisho ya dini za Mashariki ambayo kwa kiwango kikubwa huwanasa vijana. Kama haya hayatoshi, kuna ongezeko kubwa la viongozi wa kiroho wanaojiweka wenyewe badala ya kuitwa na Mungu. Mambo haya yanapingana na maagizo Mungu yanayopatikana katika kitabu cha Kumbukumbu la torati yanayosema kuwa: “Asionekane kwako mtu ampitishaye mwanawe au binti yake kati ya moto, wala asionekane mtu atazamaye bao, wala mtu atazamaye nyakati mbaya, wala mwenye kubashiri, wala msihiri, wala mtu alogaye kwa kupiga mafundo, wala mtu apandishaye pepo, wala mchawi, wala mtu awaombaye wafu. Kwa maana mtu atendaye hayo ni chukizo kwa BWANA; kisha ni kwa sababu ya hayo BWANA, Mungu wako, anawafukuza mbele yako. Uwe mkamilifu kwa BWANA, Mungu wako” (Kumbukumbu la Torati 18:10-13). Ukengeufu tulioutaja umeenea kama donda ndugu kila mahali katika mataifa yaliyoendelea na yale yanayoendelea.

Kuanzishwa upya kwa taifa la Israeli

Tayari tumeonyesha umuhimu wa taifa la Israeli katika usitawi na maendeleo ya wanadamu wote. Kuanzishwa tena kwa taifa la hili hakukuwa tu kwa maana kwa taifa la Israeli, bali ilikuwa pia ni ishara ya kuvutia inayoashiria kukaribia kwa siku ya kurudi kwa Yesu na ya hukumu ya mwisho. Zaidi ya miaka 2,500 Mungu alimpa nabii Ezekieli ujumbe ufuatao; “Tazama, nitawatwaa wana wa Israeli toka kati ya mataifa walikokwenda, nami nitawakusanya pande zote, na kuwaleta katika nchi yao wenyewe; … Katika miaka ya mwisho, utaingia nchi … juu ya milima ya Israeli, iliyokuwa ukiwa wa daima; … Itakuwa katika siku za mwisho, nitakuleta upigane na nchi yangu, ili mataifa wanijue” (Ezekieli 37:21; 38:8.16). Mwaka 1948 ulimwengu kwa mara ya kwanza ulishuhudia kurudi kwa Wayahudi kwa wingi kutoka katika pande zote za dunia, na kuingia katika nchi yao iliyofufuka tena. Baada ya kuingia katika nchi yao ilichukua miaka isiyozidi ishirini, kwa Israeli kuwa taifa mashuhuri lenye nguvu katika maswala ya kisiasa,kijeshi na kiuchumi katika eneo la Mashariki ya Kati. Sawasawa na maneno ya manabii katika Biblia, taifa hili liligeuza eneo la jangwa kuwa mashamba yenye wingi wa mazao.

Kuinuka kwa taifa la Urusi kijeshi

Unabii mwingine unaohusu siku za mwisho uliotimia ni ule ulioandikwa katika sura ya 38 ya kitabu cha Ezekieli. Maendeleo yaliyofikiwa na taifa la Urusi na umaarufu wake kijeshi, vinalingana na unabii huu. Mpaka sasa mataifa ya bara la Ulaya Magharibi na Asia yanamwangalia “Dubu wa Siberia” kwa tahadhari kubwa. Hii ni kwa sababu, kufuatana na unabii katika kitabu cha Ezekieli, katika siku siku za mwisho dubu huyu atatoka katika pango lake, ili kushindana na Simba aliye wa kabila la Yuda.

Kuongezeka kwa maarifa

Kuongezeka kwa maarifa ni jambo lingine tunalokutana nalo katika unabii wa Danieli unaohusu siku za mwisho. Katika kitabu cha Danieli tunasoma maneno yafuatayo; “Lakini wewe, Ee Danieli, yafunge maneno haya, ukakitie muhuri kitabu, hata wakati wa mwisho; wengi wataenda mbio huko na huko, na maarifa yataongezeka” (Danieli 12:4) Inavyoonekana siku hizi, maarifa ya wanadamu na elimu vimeongezeka kwa namna ya kushangaza. Kamwe hatutakosea pale tutakapoziita siku zetu kwa ni ni za sayansi na tekinolojia. Katika karne chache zilizopita mwanadamu alijishughulisha katika uvumbuzi uliozaa vitu kama ndege, roketi, simu, televisheni, tovuti, kompyuta, na utandawazi. Ujuzi na elimu vimeongezeka kiasi cha kuufanya ulimwengu uchanganyikiwe. Haijawahi kutokea wakati wowote katika historia ya wanadamu ambapo kumekuwa na ubunifu na uvumbuzi unaoenea kwa kasi kama ilivyotokea katika siku tulizo nazo.

Bomu la Atomu na silaha za Nyuklia

“Lakini siku ya Bwana itakuja kama mwivi; katika siku hizo mbingu zitatoweka kwa mshindo mkuu, na viumbe vya asili vitaunguzwa, na kufumuliwa, na nchi na kazi zilizomo ndani yake zitateketea. Basi, kwa kuwa vitu vyote hivi vitafumuliwa hivyo, imewapasa ninyi kuwa watu wa tabia gani katika mwenendo mtakatifu na utauwa, mkitazamia hata ije siku ile ya Mungu, na kuihimiza; ambayo katika hiyo mbingu zitafumuliwa zikiungua, na viumbe vya asili vitateketea na kuyeyuka?” (2 Petro 3:10-12). Unabii huu wa mtume Petro wa siku za mwisho na kuja kwa Bwana unahusishwa na kipindi cha bomu la atomu na silaha za nyuklia. Kwa ujumla kama mtu yeyote atatafakari kwa kumaanisha maneno yanayopatikana katika Biblia takatifu, mashaka na kejeli zake dhidi ya Biblia vitageuka kuwa heshima kuu.

Kununua na kuuza kwa kutumia namba

“Naye awafanya wote, wadogo kwa wakubwa, na matajiri kwa maskini, na walio huru kwa watumwa, watiwe chapa katika mkono wao wa kuume, au katika vipaji vya nyuso zao; tena kwamba mtu awaye yote asiweze kuuza wala kununua, isipokuwa ana chapa ile, yaani, jina la mnyama yule, au hesabu ya jina lake” (Ufunuo 13:16-17). Maandiko ya aya hizi yanahusu unabii unaohusu kipindi kitakachokuwepo kabla ya siku ya Mwisho. Kulingana na maandiko haya, unabii huu unazungumzia kuanzishwa kwa utaratibu kufanya biashara kwa kutumia njia za kielectroniki badala ya pesa taslimu. Kulingana na mfumo huu, kila mtu atapewe namba inayomhusu yeye binafsi, inayoendana na jina lake na asipokuwa na namba hiyo hataweza kununua, wala kuuza kitu chochote. Siku hizi karibu asilimia themanini hivi za shughuli za kifedha (transactions) hufanywa kwa njia hizi za kielektronic zinazohusisha matumizi ya kadi.

Kurejea kwa dola ya Rumi

Katika kitabu cha Danieli sura ya 7 na pia katika kitabu cha Yohana, tunakutana na unabii mwingine unaohusu kuanzishwa tena kwa dola ya Rumi kabla ya kuwadia kwa Siku ya Mwisho. Wanatheolojia wanahusisha unabii huu na Jumuiya ya uchumi ya Ulaya, iliyoanzishwa na mataifa machache ya Ulaya katika mkataba uliotiwa sahihi katika mji wa Rumi. Kuondolewa kwa mipaka na kuwepo kwa sarafu moja katika mataifa ya jumuiya hii, ni ishara nyingine inayolenga kuwadia kwa mwisho wa nyakati.

Kuanzishwa kwa umoja wa mataifa

Katika kitabu cha mwisho cha Biblia tunasoma juu ya kuanzishwa kwa utawala wa dunia nzima, utakaotokea wakati wa siku za mwisho.“Nikaona kimoja cha vichwa vyake kana kwamba kimetiwa jeraha la mauti, na pigo lake la mauti likapona. Dunia yote ikamstajabia mnyama yule. Wakamsujudia yule joka kwa sababu alimpa huyo mnyama uwezo wake; nao wakamsujudia yule mnyama, wakasema, Ni nani afananaye na mnyama huyu? Tena ni nani awezaye kufanya vita naye? Naye akapewa kinywa cha kunena maneno makuu, ya makufuru. Akapewa uwezo kufanya kazi yake miezi arobaini na miwili. Akafunua kinywa chake amtukane Mungu, na kulitukana jina lake, na maskani yake, nao wakaao mbinguni. Tena akapewa kufanya vita na watakatifu na kuwashinda, akapewa uwezo juu ya kila kabila na jamaa na lugha na taifa. Na watu wote wakaao juu ya uso wa nchi watamsujudia, kila mtu ambaye jina lake halikuandikwa katika kitabu cha uzima cha mwana-Kondoo, aliyechinjwa tangu kuwekwa misingi ya dunia” ( Ufunuo 13:3-8).Kuanzishwa kwa umoja wa mataifa (UNO) pamoja na miundo yake ya kijeshi, uchumi, na shirika la fedha duniani, ni moja ya dalili ya wazi ya kukaribia kwa siku ya mwisho.

Kasi ya kuhubiriwa kwa injili ya Ufalme

Yesu Kristo anasema: “Habari Njema ya ufalme itahubiriwa katika ulimwengu wote, kuwa ushuhuda kwa mataifa yote; hapo ndipo ule mwisho utakapokuja” (Mathayo 24:14; Luka 24:47; Matendo 1:8).Kuhusiana na dalili hii ni wazi kuwa kukua kwa sayansi na tekinolojia pamoja na kuenea kwa Ukristo, vimechangia kuleta mabadiliko yaliyoupata ulimwengu katika karine zilizopita. Kuwepo kwa njia za kisasa za mawasiliano kwa kiwango kikubwa kumechangia kufikiwa kwa maendeleo haya ya Umisheni wa imani ya Kikristo. Kuenea huku kwa injili ya ufalme wa Mungu dalili ya wazi inayoonyesha kukaribia kwa siku ya kurudi kwa Yesu.
MWALIMU:senior pastor Francis Mhina Ebenezer RevivalTemple

Hakuna maoni:

Unordered List

Download

Contact Us

Jina

Barua pepe *

Ujumbe *